Ni kati ya kauli zilizotolewa mjini Kigali Rwanda katika mwanzo wa juma la kuadhimisha kumbukumbu za mauaji hayo miaka 30 iliyopita.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika nchini Rwanda na nchi za nje ambako kunaishi raia wa Rwanda, yalihudhuriwa na marais wa mataifa mbalimbali akiwemo rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na manaibu rais, mawaziri wakuu, viongozi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa na viongozi wengine waandamizi kutoka ulaya, Afrika, Asia na kwengineko
Ni zoezi ambalo pia lilitawaliwa na shuhuda za kusononesha ambazo zilivuta hisia za watu hasa kutoka kwa wale walionusurika mauaji hayo
Ayinkamiye Louse aliyenusurika mauaji hayo akiwa na miaka kumi na mmoja, alikuwa ni miongoni mwa mamia ya Watutsi waliokimbilia katika kanisa la Nyange wilayani Ngororero kusini mwa Rwanda lakini baadaye kanisa hilo likavunjwa na watu wote wakauawa.
"Ilitolewa amri ya baba paroko Athanase Seromba kuhakikisha jingo zima la kanisa tulipokuwa tumekimbilia linabomolewa na kuwekwa chini ili ahakikishe watutsi wote waliokuwa wamekimbilia wanauawa, kanisa lilivunjwa na maisha ya ndugu wote yakaishia hapo," alisema.
Ni shuhuda ambazo zilionekana kuwafanya baadhi ya watu kudondosha machozi na kujawa na simanzi usoni kulingana na uzito wake
Wawakilishi wa umoja wa ulaya pamoja na mwakilishi wa umoja wa Afrika wote wamekiri kwamba jamii ya kimataifa ilishindfwa kusimama na kuzuia mauaji hayo licha ya taarifa za kile kilichotarajia kutokea.
Mwakilishi wa umoja wa ulaya Charles Michel na raia wa Ubelgiji nchi iliyopoteza walinda Amani wake 10 nchini Rwanda wakati wa mauaji hayo kwa mara nyingine tena ameonekana kunyenyekea
"Nasikitishwa na mzizi wa historia hii na lakini pia nikiwa pia nikiwa na aibu mimi kama raia wa Ubelgiji na mtu kutoka bara la ulaya ambalo lilikuwa na uwezo pamoja na nchi yangu lakini sote tulishindwa kufanya lolote kuyasimamisha mauaji haya," alisema.
Hotuba zilizotolewa zimekuwa za kuwasutia kidole viongozi kwa kushindwa kuchukua hatua kuokoa maisha ya raia wa kitutsi waliokuwa wakiuawa mbele za macho ya kimataifa, mkuu wa kamisheni ya umoja wa Afrika Musa Faki Mahamat akahoji pia
"Vipi na kwa nini, ilikuwaje, ikawa kwamba kunawezekana kumaliza maisha yaw engine kwanini? Tunaendelea kuhoji ilikuwaje? Kwa nini? Dunia ilikuwa wapi?" aliuliza Mahamat.
Miaka 30 imepita lakini Rais Paul Kagame kuonekana kama anafafanua mzizi wa tatizo ukiendelea kuwepo hasa ukanda wa maziwa makuu. Rais Kagame amesema wanamgambo wa Kihutu wa FDLR waliofanya mauaji hayo na kukimbilia mashariki mwa DRC wanaendelea kuwa tishio.
Kagame alisema: "Majeshi ya wauaji yalipokimbilia Zaire ya zamani ambayo sasa hivi ni DRC kwa msaada wadau wao kutoka nchi waliendelea kupanga mashambulizi dhidi ya Rwanda ili kurudi na kukamilisha mauaji hayo kuwepo kwao kule mashariki mwa DRC hadi kumesababisha maelfu ya raia wa kitutsi kule DRC kukimbilia Rwanda na mataifa mengine na mpaka sasa wamesahaulika kwa miaka 30."
Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton ambaye wakati wa uongozi wake kama Rais wa Marekani analaumiwa kutofanya lolote kuyasimamisha mauaji hayo alikuwepo.
Hata hivyo nchi za Nigeria, Jamhuri ya Zcech pamoja na News Zealand zimepongezwa kwa mara nyingine tena kutokana na ujasiri wa mabalozi wao katika baraza la usalama la umoja wa mataifa kusimama na kukemea huku wakitaja kilichokuwa kikiendelea Rwanda yalikuwa ni mauaji ya kimbari.
Forum