Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 18:40

Naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua aondolewa na baraza la seneti


PICHA YA MAKTABA: Aliyekuwa naibu wa rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.
PICHA YA MAKTABA: Aliyekuwa naibu wa rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.

Bunge la seneti nchini Kenya Alhamisi lilipiga kura na kuidhinisha kuondolewa ofisini kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua,  kutokana na mashtaka 5 kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake, katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Maseneta 54 kati ya 67 walipiga kura ya kumfukuza Gachagua kwa shtaka la kwanza la "ukiukaji mkubwa wa katiba", zaidi ya theluthi mbili ya idadi inayohitajika kisheria, na kumfanya kuwa naibu rais wa kwanza kulazimishwa kuondoka madarakani kwa mashtaka kama hayo.

Ni hatua ambayo baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanasema huenda ikaitumbukiza nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika mzozo wa kisiasa.

Bunge la Kitaifa lilipiga kura wiki jana kumshtaki Gachagua, ambaye alimsaidia Rais William Ruto kushinda uchaguzi miaka miwili iliyopita lakini ameshambuliwa na washirika wa rais kwa madai ya kukosa uaminifu na msururu wa maoni ya uchochezi ya umma.

“Kulingana na hilo, Mheshimiwa Rigathi Gachagua... anakoma kushikilia wadhifa huo,” alisema Spika wa Seneti Amason Kingi.

Mchakato huo hata hivyo, hautakomea hapo. Gachagua amewasilisha maombi kadhaa kupinga shinikizo la kumtimua mamlakani, na jaji mkuu ameteua jopo la majaji watatu kusikiliza hoja zilizowasilishwa.

Gachagua, ambaye amekanusha madai hayo, alipaswa kujitetea dhidi ya mashtaka katika Seneti Alhamisi alasiri kabla ya upigaji kura. Alipokosa kufika, wakili wake Paul Muite alisema naibu huyo wa rais alikuwa amelazwa hospitalini akiwa na maumivu makali ya kifua, na kuitaka Seneti kusitisha shughuli kwa siku kadhaa.

Lakini seneti ilikataa kufanya hivyo, na kupelekea timu ya wanasheria wa Gachagua kupinga hatua hiyo na kuondoka bungeni.

Dan Gikonyo, daktari anayemtibu Gachagua, aliwaambia wanahabari kuwa mwanasiasa huyo alilazwa katika hospitali ya Nairobi akiwa na tatizo la moyo Alhamisi mchana, lakini sasa yuko sawa na kuna uwezekano atalazimika kusalia hospitalini kwa saa 24-72.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, rais ana uhuru wa kumteua naibu mwingine baada ya seneti kuchukua hatua kama hiyo.

Maseneta wakisikiliza hoja katika baraza la seneti mjini nairobi, Kenya.
Maseneta wakisikiliza hoja katika baraza la seneti mjini nairobi, Kenya.

Baadhi ya maseneta walitilia shaka uamuzi wa kuendelea na kura, licha ya kutokuwepo kwa Gachagua.

"Tunapaswa kumwondoa madarakani mtu akiwa hospitalini kwa sababu uhalifu pekee ambao Rigathi Gachagua ametenda ni uhalifu wa kisiasa, kwa hivyo inabidi aondolewe kwa mbinu yoyote ile?" aliuliza Seneta wa Kkaunti ya Nyandarua, John Methu.

Lakini Seneta Moses Otieno Kajwang alitetea hatua ya kumshtaki Gachagua akisema, "lazima tuodoe wahalifu kati yetu".

HATARI KWA RUTO

Ruto, ambaye alitofautiana na Gachagua katika miezi ya hivi karibuni, hajazungumza lolote kuhusu kesi hiyo, lakini huenda akakabiliwa na upinzani wa umma kufuatia kuondolewa madarakani kwa Gachagua, wachambuzi wa masuala ya kisiasa walisema.

Wakenya wengi wanaona mchakato wa kumtimua kama uliochochewa kisiasa, kufuatia matokeo ya maandamano mabaya ya kupinga ushuru mnamo Juni na Julai ambayo yalifichua kutoridhika na sera za serikali na madai ya ufisadi.

Gachagua, ambaye hapo awali alitaja mchakato wa kumtimua kuwa ni njama za kisiasa zinazozingatia madai ya uwongo, alipaswa kujibu msururu wa shutuma zilizotolewa Jumatano na mbunge Mwengi Mutuse, ambaye alimshutumu kwa kuchochea chuki za kikabila.

Mutuse pia alimshutumu Gachagua kwa kupata mali yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 40 tangu awe naibu rais, licha ya kuripoti utajiri wa takriban dola milioni 6 pekee kabla ya kuingia ofisini. Elisha Ongoya, mwanachama wa timu ya wanasheria wa Gachagua, alisema madai hayo hayana ushahidi na yalitokana na uvumi.

Forum

XS
SM
MD
LG