Katika mojawapo ya mikataba iliyotarajiwa sana, wawekezaji kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) walijitolea kununua hati za kaboni za dola milioni 450 kutoka Mpango wa Masoko ya Kaboni Afrika (ACMI) ambao ulizinduliwa katika mkutano wa kilele wa COP27 wa Misri mwaka jana.
Viongozi wa Afrika wanaunga mkono mipango ya ufadhili, kama vile hati za kaboni, ambazo zinaweza kutokana na miradi inayozuia uzalishaji wa gesi chafuzi, hususan katika nchi zinazoendelea, kama vile kupanda miti, au kubadili nishati safi.
Hati za kaboni zinaweza kununuliwa na makampuni ili kukabiliana na uzalishaji ambao hawawezi kukata kutoka kwa shughuli zao wenyewe ili kusaidia kufikia malengo ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Waandalizi wa mkutano huo wa siku tatu mjini Nairobi wanasema wanalenga kuonyesha Afrika kama kivutio cha uwekezaji wa hali ya hewa badala ya kuwa mwathirika wa mafuriko, ukame na njaa.
Serikali za Afrika zinaona hati za kaboni na vyombo vingine vya ufadhili vinavyotegemea soko kuwa muhimu katika kutafuta ufadhili ambao umekuwa polepole kutoka kwa mataifa tajiri duniani, ambao umekuwa ukipatika kwa kasi ndogo.
Katika hotuba yake kwa kikao cha ufunguzi rais wa Kenya, William Ruto amesema wakati umefika kwa bara la Afrika kutafuta ufumbuzi wa athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Ruto amewataka wajumbe wa mkutano huo kutumia mkutano huo wa siku tatu kutathmini mitazamo, na kutafuta suluhu na kubuni mikakati ya kubadilisha utajiri wa rasilimali za Afrika kutoka kwa uwezo hadi kuwa fursa halisi, kwa kuelekeza uwekezaji mkubwa ambao utafanikisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Hatua chache kutoka ukumbi wa mkutano, wanaharakati wa mashirika ya kiraia wamekuwa wakifanya maandamano sambaba na mkutano huo, wakiomba kujumuishwa kwa jamii zilizoathirika zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa.
Forum