Baraza la Kitaifa la Viongozi wa Kidini la Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo CENCO, linalosimamia upatanishi kati ya serikali na upinzani, litawasilisha Alhamisi pendekezo la kutanzua mzozo wa kisaisa nchini humo.
Georges Kapiamba, mwakilishi wa asasi za kiraia akiwa moja wapo wa wajumbe 16 wa tume ya majadiliano kati ya serikali na upinzani ameiambia Sauti ya Amerika kwamba, Maaskofu wa Kanisa la Katholiki, wanadhani wana pendekezo la kutanzua mzozo uliyopo.
Hadi hivi sasa tofauti kuu iliyopo ni juu ya mamlaka ya Rais Joseph Kabila wakati wa kipindi cha mpito, baada ya muda wake rasmi kumalizika hapo Disemba 19.
Vyama vikuu vya upinzani vilivyoungana chini ya jina jipya la Rasemblement walosusia mazungumzo yaliyoongozwa na Umoja wa Afrika, wanataka serikali ya mpito ikiwa itaongozwa na Kabila au la ni lazima ipunguze sana madaraka ya kiongozi huyo.
Halikadhalika upinzani unataka uchaguzi ufanyike mnamo mwaka ujao wa 2017, huku serikali na baadhi ya vyama vya upinzani vinataka uchaguzi ufanyike 2018.
Bw Kapiamba, akiwa katika tume maalum ya majadiliano anasema ana matumaini kwamba pande zote zitaweza kufikia makubaliano kabla ya sikukuu ya Krismasi kama vile Maskofu wanavyotaka.
Bank Ki-moon atoa wito
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ametoa wito Jumatano jioni kwa wadau wote huko Kongo, kuhakikisha wanafikia makubaliano katika mazungumzo yanayoongozwa na viongozi wa kidini.
Katika taarifa yake Bw. Ban amesisitiza kwamba "kupunguza mvutano na kubuni mazingira yanayostahiki ya kufanikiwa majadiliano yanayosimamiwa na Cenco katika muda mfupi uwezekanavyo ni muhimu, pamoja na kutayarisha uchaguzi wa kuaminika na wazi".
Katibu Mkuu alilaani pia vifo vilivyotokea Jumatatu na jumanne wakazti wa ghasia baada ya muda wa muhula wa pili wa Kabila kumalizika. Maandamano katika miji mbali mbali ya kongo yalikandamizwa na polisi na kiusababisha vifo vya karibu watu 19