Afrika Kusini: Zuma akanusha tuhuma za rushwa

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.

Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, ambaye utawala wake uligubikwa na sakata mbalimbali Jumatatu aliliambia jopo la mahakama linalochunguza madai ya rushwa dhidi yake kuwa kuna njama inayolenga kumuonyesha kama "mfalme wa ulaji rushwa."

Aidha mwanasisa huyo alisema kuna njama ya kumuangamiza kisiasa. Zuma alishangiliwa na wafuasi wake alipokaribia jengo ambako jopo hilo linakutana.

Ilikuwa mara yake ya kwanza kufika mbele ya jopo hilo.

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 77, alilazimishwa kujiuzulu wadhifa wa urais wa mwezi Februari mwaka 2018 kufuatuia tuhuma za ufisadi wa hali ya juu uliodaiwa kutekelezwa naye kwa ushirikiano na maafisa wa chama tawala cha African National Congress (ANC).

Akijitetea, Zuma aliliambia jopo hilo, linaloongozwa na jaji Raymond Zondo, kwamba madai hayo ya ufisadi ni njama ambayo imekuweko kwa muda mrefu inayokusudiwa kumchafulia jina.

Alidai kuwa mpango huo unatekelezwa na wakuu wa chama cha ANC, wakiwa na madhumuni ya kumuondoa kwenye siasa za taifa hilo la Kusini mwa Afrika.