Rais wa Afrika Kusini anayekabiliwa na kashfa, Jacob Zuma amejitetea katika mahojiano Jumatano, akisema shinikizo linalomtaka yeye kujiuzulu “si haki” na kwamba hajafahamishwa kosa lake ni nini.
Akizungumza na shirika la utangazaji la taifa SABC, Zuma amesema amekutana na maafisa wa ngazi ya juu wa Chama tawala cha ANC mwisho wa wiki iliopita na wamekubaliana na kile alichosema ni kuchelewesha kwake kujiuzulu.
Amesema amependekeza kubakia madarakani hadi mwezi Juni 2018. Lakini viongozi wa ANC wamekataa mpango huo na kumtaka Zuma kuachia madaraka mara moja.
Chama kimesema kuwa bunge litapiga kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Zuma Alhamisi, iwapo rais hatokubali kuachia madaraka mara moja.