Rais wa Marekani, Barack Obama, anakutana na Rais Mauricio Macri mjini Buenos Airies, mji mkuu wa Argentina akianza ziara ya siku mbili ambayo inaashiria uhusiano mzuri kati ya mataifa haya mawili.
Rais Obama aliwasili Buenos Aires mapema leo baada ya kumaliza ziara yake ya kihistoria ya Cuba ambako amesema amezika ukurasa wa mwisho wa vita vya baridi.
Usalama umeimarishwa katika mji mkuu kufuatia mashambulio ya Jumanne mjini Brussels, mji mkuu wa Ubelgiji. Baadhi ya vituo vya usafiri wa treni na barabara karibu na mahala Obama atatembelea zimefungwa.
Rais Macri, aliyechukua madaraka mwezi Disemba amedokeza kwamba anataka ushirikiano wa karibu wa kiuchumi na Washington na mataifa mengine makuu ya kiuchumi.
Ziara ya Obama inafanyika wakati wa kuadhimisha miaka 40, siku ya Alhamisi, ya kuanza kwa utawala wa kikatili wa kimabavu huko Argentina iliyopelekea vifo au kutoweka karibu watu 30,000.
Mke wa Rais mama Michelle Obama yupo pamoja naye wakiambatana na mabinti wao wawili.