John Kerry: Ni fahari kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry akiongea na waandishi wa habari mwishoni mwa mikutano ya G7 huko Hiroshima, Japan.

John Kerry anasema anajivunia heshima kubwa ya kuwa waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Marekani kutembelea Hiroshima, nchini Japan - mji ambao uliharibiwa baada ya Marekani kuangusha bomu moja la atomiki karibu na mwishoni mwa vita vya pili vya dunia.

Bwana Kerry alitoa matamshi hayo mwishoni mwa mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la G7 ambayo ilijumuisha ziara ya kumbukumbu ya waathirika wa vita vya pili vya dunia huko Hiroshima.

Alipoulizwa kama rais Obama atatembelea Hiroshima wakati anapohudhuria mkutano wa viongozi wa G7 nchini Japan mwezi mei, Kerry alisema anamatumaini kwamba siku moja rais wa Marekani atakuwa miongoni mwa watu ambao wameutembelea mji huo. Aliongeza kwamba Rais Obama alielezea nia ya kutembelea huko lakini hajui kama ratiba ya rais itamruhusu kufanya hivyo wakati wa ziara yake ijayo nchini Japan.