Ziara ya Biden ya California yasitishwa ghafla kutokana na upepo hatari

  • VOA News

Wafanyakazi wakiondoa ubao uliyoangushwa na upepo mkali wakati wa ziara ya rais wa Marekani Joe Biden ya bonde la Eastern Coachella ,California. Jan 7 , 2024

Upepo mkali na hatari Jumanne ulimlazimisha rais wa Marekani Joe Biden kufuta ziara yake kwenye bonde la Eastern Coachella, ambapo alikuwa atangaze makaburi mawili mapya ya kitaifa ya kumbukumbu ya wazawa wa Marekani huko California.

Upepo ulianza kushika kasi kote kusini mwa California wakati wataalam wa hali ya hewa wakionya “kuwa ni tishio kwa maisha.” Tayari Biden alikuwa ameingia kwenye gari lake rasmi kuanza safari, wakati tukio hilo lilipofutwa.

White House awali ilisema kuwa Biden angehutubia akiwa Los Angeles, lakini baadaye ilitangazwa kuwa itafanyika wiki ijayo huko Ikulu, ikiwashirikisha watu wengine pia. Idara ya Kitaifa ya Hali ya Hewa imesema kuwa upepo huo wa Santa Ana, ndiyo wenye nguvu zaidi kwa zaidi ya muongo mmoja, na kwamba utashika kasi zaidi Jumatano asubuhi, ukikisiwa kuwa katika kasi ya kilomita 129 kwa saa.

Baadhi ya maeneo ya milima na mabonde huenda yakashuhudia upepo wa kasi ya hadi kilomita 160 kwa saa. Tangazo la Biden ni sehemu ya utawala wake ya kuhifadhi takriban asilimia 30 ya ardhi ya Marekani pamoja na maji ifikapo 2030, kupitia mpango wake wa ‘America the Beautiful.”