Zelenskyy: Tutashinda Russia mwaka huu 2023

Rais wa Ukrain Volodymyr Zelenskyy akiwa amebeba bendera ya kijeshi huku mwanajeshi akiipiga busu wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa uvamizi wa Russia. Feb. 24, 2023.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameahidi kwamba nchi yake itapata ushindi dhidi ya Russia mwaka huu wa 2023.

Amesema hayo wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja tangu Russia ilipovamia Ukraine kijeshi Februari 24 mwaka uliopita.

Zelenskyy amesema siku Russia ilivamia nchi hiyo, ilikuwa siku ndefu sana kwa Maisha ya raia wa Ukraine, lakini nchi hiyo imefanikiwa kisimama imara na kupambana na kwamba wataendelea kupambana.

Katika maadhimisho yaliyojaa huzuni, rais Zelenskky ameonyesha ujasiri kwa watu wake na kuendelea kupambana na Russia katika vita hivyo vibaya kuwahi kutokea tangu vita vya pili vya dunia.

Amesema kwamba raia wa Ukraine wamedhihirisha kwamba hawawezi kutishwa, na wenye Imani na umoja licha ya mwaka uliojaa uchungu, na huzuni.

Mamilioni ya watu wamekoseshwa makao, mamilioni wanahitaji msaada, maelfu wameuawa wakiwemo wanajeshi, na mali kuharibiwa katika vita hivyo.

Vikwazo zaidi dhidi ya Russia na washirika wake

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskky, amesema kwamba nchi yake itashinda uvamizi wa Russia, wakati vita hivyo vikiingia mwaka wa pili bila kuwepo ishara ya kumalizika.

Zelenskyy amesema kwamba Ukraine imestahmili, na haijashindwa na kwamba watafanya kila liwezekanalo kupata ushindi mwaka huu, akiongezea kwamba Ukraine imetoa motisha na kuunganisha dunia.

Viongozi wa nchi 7 tajiri duniani wanakutana leo ijumaa, na wanatarajiwa kutangaza vikwazo vipya dhidi ya watu na mashirika yanayoIsaidia Russia katika uvamizi wake nchini Ukraine.

White House imesema kwamba itaweka vikwazo kadhaa ikilenga benki, sekta za madini na ulinzi, pamoja na zaidi ya watu 200 na mashirika.

Vikwazo vitatolewa dhidi ya watu na mashirika kote Ulaya, Asiam na Mashariki ya Kati.

Marekani imetangaza msaada wa kijeshi wa dola bilioni 2 kwa Ukraine. Msaada huo pia unajumuisha mfumo wa ulinzi wa anga na wa kurusha makombora.