Zelenskyy atembelea Kherson baada ya wanajeshi wa Russia kuondoka

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akikitana wa wanajeshi wake mjini Kherson, Jumatatu. Nov 11, 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiyy Jumatatu amewahutubia wanajeshi wake kwenye mji wa Kherson uliokombolewa kutoka mikononi mwa Russia, akisema kwamba taifa lake lipo tayari kwa amani.

Ziara ya Zelenskyy imekuja siku chache tu baada ya vikosi vya Russia kuondoka kwenye mji huo uliopo kusini mwa nchi. Wizara ya ulinzi ya Uingereza kupitia ujumbe wa Twitter imesema kwamba msimu wa baridi utaleta mabadiliko kwenye operesheni za vikosi vya Russia na Ukraine vinavyoshiriki kwenye mapigano ya Ukraine.

Zelenskyy wakati wa ziara ya Kherson amewakumbusha wakazi kwamba hali bado ni ya hatari kwa kuwa kuna mabomu yaliyotegwa ardhini, na hivyo kuwaomba kuwa waangalifu. Maafisa wa Ukraine Jumapili wameanza kupeleka misaada muhimu mjini humo ,ikiwemo chakula, maji na dawa, zikiwa siku mbili tu baada ya vikosi vya Russia kuondoka, baada ya kuushikilia mji huo tangu mwanzoni mwa vita hivyo.