Zelenskyy amesema katika ujumbe wa Twitter, “kwa muda mrefu, Russia ilitumia propaganda kuficha udhaifu wake na upuuzi wa serikali yake. Na sasa kuna machafuko mengi sana ambayo hakuna uwongo unaoweza kuificha.”
Majibu hayo yanafuatia pia taarifa ya rais Vladimir Putin kuapa kwamba atawaadhibu wasaliti wa kundi la wamamluki wa Wagner kufuatia uwasi huo na baada ya kiongozi wa kundi hilo kuapa atapindua uwongozi wa kijeshi wa Moscow.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alituma ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa, akiitaka iachane na kile alichokiita “kutoegemea upande wowote” kuhusu Russia na kuipatia Ukraine silaha inayohitaji kujilinda dhidi ya uvamizi wa Russia.
Ikulu ya White House ilisema inafuatilia mzozo kati ya maafisa wakuu wa jeshi la Russia, na jeshi la Wagner na itashauriana na washirika na wadau kuhusu maendeleo, msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa, Adam Hodge aliiambia VOA Ijumaa.