Zelenskyy anaomba hatua ichukuliwe kuipatia Ukraine misaada ya kijeshi

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy

Jeshi la anga la Ukraine limesema ulinzi wa anga wa nchi hiyo ulitungua ndege 39 kati ya 40 zisizokuwa na rubani

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy leo Alhamisi ameomba hatua ichukuliwe kuipatia nchi yake misaada ya kijeshi hasa mifumo ya ulinzi wa anga baada ya usiku wa mashambulizi ya anga ya Russia ambayo jeshi la Ukraine lilisema yalijumuisha makombora 42 na ndege zisizokuwa na rubani 40.

Kama makombora ya Russia na ndege zisizo na rubani aina ya “Shahed” zinaendelea kushambulia sio tu Ukraine lakini pia azimio la washirika wetu, hii itaongeza leseni ya kimataifa ya ugaidi, Zelenskyy alisema kwenye mitandao ya kijamii. Tunahitaji mifumo ya ulinzi wa anga na misaada mingine ya ulinzi, sio tu kufumbia jicho na kuwa na majadiliano marefu.

Zelenskyy alisema mashambulizi ya hivi karibuni yalilenga mikoa ya Kharkiv, Kyiv, Zaporizhzhia, Lviv na Odesa. Magaidi wa Russia kwa mara nyingine tena wamelenga miundombinu muhimu, Zelenskyy alisema. Jeshi la anga la Ukraine limesema ulinzi wa anga wa nchi hiyo ulitungua ndege 39 kati ya 40 zisizokuwa na rubani na kuharibu makombora 18 kati ya 42.

Kampuni ya umeme ya Ukraine Ukrenergo imesema mashambulizi ya Russia yaliharibu vituo vyake vya umeme katika mikoa mitano tofauti.