Zaidi ya watu 6 wafariki katika mkanyagano kwenye michuano ya AFCON

Mashabiki wa michuano ya AFCON

Maafisa wa Cameroon wamesema kwamba takriban watu 6 wamekufa baada ya mkanyagano nje ya uwanja mmoja wa mpira kunakofanyikia michuano ya kombe la Afrika la AFCON.

Kwa mujibu wa shirika la Habari la Associated Press, Gavana wa jimbo la katikati mwa Cameroon Naseri Biya ameongeza kusema kwamba idadi hiyo huenda ikaongezeka.

Mkanyagano huo unasemekana kutokea baada ya watu kusongamana wakijaribu kuingia kwenye uwanja wa mpira wa Olembe mjini Yaounde, ili kutazama mechi kati ya Cameroon na Comoros.

Maafisa wa afya kutoka hospitali iliyo karibu na uwanja huo ya Massassi wamesema kwamba walipokea takriban watu 40 waliojeruhiwa kwenye mkasa huo.

Maafisa wamesema kwamba takriban watu 50,000 walikuwa wakijaribu kuingia kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kubeba watu 60,000 wakati ukiruhusiwa kuwa na asilimia 80 pekee ya watu kwa wakati mmoja, kutokana na kanuni za kujiepusha na maambukizi ya corona.

Cameroon hata hivyo ilishinda kwenye mechi hiyo kwa 2-1 dhidi ya Comoros na kwa hivyo kufuzu kuingia robo fainali.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limesema kuwa kuna tukio limetokea na kwamba wanajaribu kupata taarifa zaidi.

"CAF kwa sasa inachunguza hali hiyo na kujaribu kupata maelezo zaidi juu ya kile kilichotokea," taarifa yao ilisoma.

"Tuko katika mawasiliano ya mara kwa mara na serikali ya Cameroon na kamati ya maandalizi," alisema,

"Leo usiku rais wa CAF, Dk Patrice Motsepe, alimtuma Katibu Mkuu, Véron Mosengo-Omba, kuwatembelea majeruhi katika hospitali ya Yaoundé."

Uwanja wa Olembe una uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 lakini, kutokana na kanuni za Covid-19, mamlaka zilipunguza idadi hiyo hadi asili mia 80, ambayo ni takriban mashabiki 48,000.

Cameroon ilishinda mechi hiyo mabao 2-1 na sasa watakuwa wenyeji wa Gambia katika robo fainali siku ya Jumamosi.

Mechi hiyo itafanyika mjini Douala lakini, na iwapo Cameroon watashinda, watakuwa kwenye nafasi ya kucheza nusu fainali na fainali, inayoweza kuchezwa katika uwanja wa Olembe.

Wachezaji wa timu ya Cameroon washangilia ushindi dhidi ya Comoro.

Uwanja huo pia ulitarajiwa kuwa mwenyeji wa robo fainali siku ya Jumapili kati ya mshindi wa mechi kati ya Ivory Coast na Misri na ile ya Morocco na Malawi.

Lakini sasa kufuatia mkasa huo, maswali mazito huenda yakaulizwa juu ya uwezo wa uwanja huo kustahimili watu wengi katika kipindi kilichosalia cha dimba hilo.