Zaidi ya watu 2,500 wameuwawa au kujeruhiwa katika ghasia za magenge nchini Haiti kuanzia Januari hadi Machi, zikiwa zimeongezeka kwa asilimia 53 katika miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2023, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haiti (BINUH) imeeleza.
Takriban 590 waliuwawa wakati wa operesheni za polisi, BINU imesema katika ripoti.
Imebainika kuna kadhaa ambao hawakuhusika katika vurugu za magenge, baadhi walikuwa na ulemavu wa viungo vya kuwazuia kutembea, na takriban 141 waliuwawa na makundi ya raia yenye hasira na kujichukulia sheria mkononi.
Ghasia nyingi zilifanyika katika mji mkuu wa Port-au-Prince, wakati takriban watu 438 wakitekwa nyara katika maeneo mengine ya nchi.
Maeneo ya bandari ya La Saline na Cite Soleil ya mji mkuu yalikuwa na mashambulizi makubwa zaidi ya muda mrefu.
Wanachama wa magenge waliendelea na vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake na wasichana katika vitongoji vya wapinzani, magerezani, na kambi za wakimbizi ripoti hiyo imeeleza.