Zaidi ya watoto 1,200 wamefariki katika kambi za wakimbizi nchini Sudan-UNICEF

Kambi ya muda kwa Wasudan waliokimbia mzozo katika mkoa wa Darfur, ni karibu na mpaka kati ya Sudan na Chad, Mei 13, 2023. Picha ya Reuters

Zaidi ya watoto 1,200 wamefariki katika kambi za wakimbizi nchini Sudan tangu mwezi Mei, huku maelfu ya watoto wanaozaliwa huenda watakufa ifikapo mwisho wa mwaka huu, Umoja wa mataifa umesema Jumanne.

Umoja wa mataifa umetoa tahadhari hiyo kutokana na athari za mzozo wa Sudan kwa hali ya afya kwa watoto.

“Kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya kikatili bila kujali maisha ya raia ambayo yanalenga huduma za afya na lishe, UNICEF inahofia maelfu ya watoto wachanga watakufa kati ya sasa na mwishoni mwa mwaka,” msemaji wa shirika hilo la kimataifa linalohudumia watoto James Elder amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva.

Ameelezea kwamba zaidi ya watoto 300,000 wanatarajiwa kuzaliwa nchini humo kati ya Oktoba na Disemba.

Amesema, wakati huo huo huduma za lishe katika nchi hiyo inayokumbwa na vita “ziliharibiwa”.

Shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi, limesema kwamba wafanyakazi wake katika jimbo la Sudan la White Nile walibaini kuwa kati ya Mei 15 na Septemba 14, zaidi ya watoto 1,200 walio na umri wa chini ya miaka mitano walifariki katika kambi tisa za wakimbizi.