Zaidi ya washukiwa 1,000 wakamatwa na Interpol kwa uhalifu wa mitandao Afrika

  • VOA News

Watu wakitembe karibu na makao makuu ya Interpol mjini Lyon, Ufaransa.

Idara ya polisi wa kimataifa ya Interpol imesema Jumanne kwamba imekamata zaidi ya washukiwa 1,000 wa uhalifu wa kimitandao barani Afrika, wakati wa operesheni iliyochukua miezi miwili.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, operesheni hiyo kwa jina Serengeti ilihusisha tawi la Interpol la Afrika la Afripol, na ilianza Septemba 2 hadi Oktoba 13, kwenye nchi 19 za kiafrika, ikilenga wahalifu wa udukuzi, wezi wa barua pepe, na wezi wa kimitandao.

Katibu mkuu wa Iterpol, Valdecy Urquiza, amesema kuwa uhalifu wa kimitandao umeshamiri sana, suala ambalo linatia wasi wasi. Interpol ilitambua waathirika 35,000 ambao walipoteza jumla ya karibu dola milioni 193 kote duniani.

Sekta ya kibinafsi wakiwemo watoa huduma za internet walishirikiana na Interpol kwenye operesheni hiyo. Mkuu wa Afripol Jalel Chelba kupitia taarifa amesema kuwa “Kupitia operesheni ya Serengeti, Afripol wameimarisha usalama kwenye mataifa wanachama wa Umoja wa Africa.

Enrique Hernandez Gonzalez, naibu mratibu wa Operesheni ya Uhalifu wa kimitando ya Interpol ameambia AP kwamba operesheni ya Serengeti ilikuwa yenye ufanisi mkubwa zaidi kulinganashwa na za awali. Operesheni za awali za Iterpol ndani ya miaka miwili zilipelekea kukamatwa kwa watu 25 pekee.