Waziri wa ulinzi wa Israel, Yoav Gallant amemshambulia waziri mkuu Benjamin Netanyahu kwa kushindwa kubuni mpango wa kuitawala Gaza baada ya kumalizika kwa vita vya Israel na Hamas.
Lakini kiongozi huyo wa Israel alisema kuwa haina maana kufanya hivyo hadi wanamgambo watakaposhindwa. Katika mvutano usio wa kawaida kati ya viongozi hao wawili, Gallant alisema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni kwamba anapinga kuanzishwa kwa jeshi la Israel au udhibiti wa kiraia mdogo katika Ukanda wa Gaza kwenye bahari ya Mediterania ambako ni makazi ya Wapalestina milioni 2.3.
“Tangu Oktoba, nimekuwa nikizungumzia suala hili mara kwa mara katika Baraza la Mawaziri, na sijapata majibu”, Gallant alisema. “Ninatoa wito kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kufanya uamuzi na kutangaza kwamba Israel haitaanzisha udhibiti wa raia katika Ukanda wa Gaza,” Gallant alisema, akitoa wito wa “utawala mbadala kwa Hamas.”