Serikali ya yemen imetoka katika mazungumzo ya amani baina yake na waasi wa Houthi yaliyodhaminiwa na umoja wa mataifa.
Waziri wa mambo ya nje wa Yemen Abdul –Malik Mekhlafi ameyaita mazungumzo yanayofanyika kuwa ni kupoteza muda. Amesema waasi wa Houthi wanasisitiza kuwepo na ushirikiano wa madaraka badala ya kufuata makubaliano katika baraza la usalama yanayosema kwamba masuala kama hayo lazima yafanyiwe mashauriano na kukubaliana.
Waziri huyo ameshutumu kundi la Houthi kwa kukiuka sitisho la mapigano huko Yemen na kutumia mazungumzo kama fursa ya kuendelea na msimamo wao.
Waasi bado hawajajibu kuhusu hatua ya serikali ya Yemen kutoka katika mazungumzo ya amani.
Waasi wa Houthi wanaungwa mkono na Iran walichukua udhibiti wa mji mkuu wa Sanaa mwaka 2014 na kulazimisha serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa kwenda Saudi Arabia kabla ya kurejea na kujipanga katika mji wa bandari wa Aden.
Mapigano ardhini huko Yemen pamoja na yale ya anga yanayoongozwa na Saudi Arabia yamesababisha hali mbaya ya kibinadamau , huku umoja wa mataifa ukisema kuwa asilimia 80 ya raia wa Yemen wanauhitaji mkubwa wa chakula na msaada wa kiafya.