Rais wa muda mrefu wa Gambia Yahya Jammeh amesema ni Mungu pekee anayeweza kumnyima ushindi wake wakati akijitahidi kubatilisha matokeo ya uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu. Kiongozi wa upinzani Adama Barrow alimshinda Jammeh kwenye uchaguzi wa Desemba mosi.
Mwanzoni rais huyo alikubali kushindwa lakini akabatilisha msimamo wake kwa madai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na dosari na kuomba mahakama kuu kubatilisha matokeo hayo. Kupitia televisheni ya kitaifa Jumatano Jammeh alisema “sitakandamizwa na nguvu zozote ulimwenguni, nitahakikisha haki inatendeka mimi ni mtu wa amani lakini si mwoga pia’’.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika pamoja na Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi Ecowas wote wamemuomba Jammeh kukubali kushindwa na kumuachia Barrow mamlaka.
Mahakama kuu ya nchi hiyo imepanga January 10 mwakani siku ya kusikiliza kesi ya Jammeh ikiwa ni siku 9 kabla ya muda anaotakiwa kukabidhi mamlaka.