Xiomara Castro aapishwa kuwa rais wa Honduras

Rais Xiomara wakati wa kuapishwa

Xiomara Castro Alhamisi ameapishwa kama rais wa kwanza mwanamke wa Honduras, kwenye hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya watu waliokuwa wakipeperusha vibendera vya taifa hilo kwenye uwanja wa kitaifa kwenye mji mkuu wa Tegucigalpa.

Castro ameshika usukani wa taifa hilo wakati kukiwa na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa ajira, ufisadi, ghasia za mara kwa mara, mifumo mibovu ya afya na elimu, pamoja na shinikizo kutoka Marekani la kuboresha hali ya maisha ya watu wa Honduras, ili kuwazuia kufanya safari hatari ya kaskazini kupitia Mexico wakijaribu kufika hapa Marekani.

Miongoni wa watu mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo ni makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris. Harris katika siku za nyuma alitwikwa jukumu na rais Joe Biden la kuchunguza kiini cha watu kutoka mataifa ya amerika ya kati kama Honduras, Guatemala na El Salvador kujaribu kutorokea Marekani. Harris alitarajiwa kufanya kikao cha moja kwa moja na Castro muda mfupi baada ya kuapishwa kwake kama rais wa Honduras.