Xi anakuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi nchini China baada ya Mao Zadong.
Kiongozi wa chama cha Kikomunisti Li Qiang, amekuwa kwenye jukwaa moja na rais Xi wakati wa kuzinduliwa kwa wanachama wa kamati ya juu ya uongozi wa China, na hivyo kumuweka katika nafasi nzuri ya kuwa waziri mkuu wakati Li Keqiang atakapostaafu mwezi Machi.
Wanachama wengine wa kamati hiyo ya watu saba ni pamoja na Zhao Leji na Wang Huning, ambaye amehudumu katika kamati ambayo muda wake ulimalizika.
Wengine ni Cai Qi Ding Xuexiang na Li Xi.
Wachambuzi wa siasa za China wanasema wanakamati wote ni watu wenye uhusiano mzuri sana na rais Xi, ambaye ameiongoza China kwa njia ya kibabe tangu alipoingia madarakani mwaka 2012.
Richard McGregor, mtaalam wa maswala ya Asia anasema kwamba matokeo hayo ni ushindi mkubwa kwa rais Xi.
"Washindani wake wote wamelazimika kuondoka kwenye kamati ya maamuzi ya juu na watu wenye ushirikiano mzuri na Xi kuchukua nafasi hizo. Hii ni ishara kwamba Xi anakidhibithi kabisa chama hicho.”
Kutangazwa kwa kamati hiyo kumefanyika siku moja baada ya chama cha kikomunisti kufunga kongamano lake la awamu ya 20 ambapo kanuni za chama zilifanyiwa mabadiliko na kutoa mamlaka zaidi kwa rais Xi kuwa mshauri mkuu wa kisiasa wa chama.
Xi, mwenye umri wa miaka 69, hata hivyo anakabiliwa na changamoto za kiuchumi wakati China ikirekodi kiwango cha chini cha ukuaji, uchumi pamoja na utekelezaji wa sera yake ya kumaliza kabisa maambukizi ya virusi vya Corona.
China pia inakabiliwa na shinikizo kali kutoka kwa mataifa ya Magharibi, kutokana na hatua yake ya kumuunga mkono rais wa Russia Vladimir Putin, pamoja na kuongezeka kwa hali ya wasiwasi kuhusu umiliki wa kisiwa cha Taiwan.