Ratiba iliyofanyika mjini Moscow Ijumaa imezigawa nchi 32 katika fainali hiyo kwenye makundi manane. Nigeria na Morocco zinaonekana kuwa katika makundi magumu zaidi kuliko nchi nyingine za Afrika.
Nigeria ipo katika kundi D ambalo linaweza kuchukuliwa kama kundi gumu zaidi likiwa na Croatia, Iceland na mabingwa wa zamani Argentina. Morocco ipo katika kundi B pamoja na Spain, Ureno na Iran.
Misri pia ipo katika wakati mgumu kwa kuwa katika kundi A ambalo lina wenyeji Russia, Uruguay na Saudi Arabia. Senegal ipo kundi H ambapo itapambana na Poland, Colombia na Japan, wakati Tunisia itakuwa katika kundi G lenye timu za Uingereza, Ubelgiji na Panama.
Mabingwa watetezi Ujerumani wako katika kundi F lenye timu za Mexico, Sweden, na South Korea wakati Brazil - siku zote wanapewa nafasi ya kuchukua kombe hilo - wapo katika kundi E lenye timu za Switzerland, Costa Rica na Serbia.
Fainali za kombe la dunia 2018 zitaanza Juni 14 na kuchukua mwezi mzima hadi Julai 15. Jumla ya mechi 64 zitachezwa katika viwanja 12 vilivyo katika miji 11 tofauti nchini Russia. Wenyeji Russia watafungua dimba na Saudi Arabia katika mechi ya kwanza kwenye uwanja wa Luzhniki, Moscow.
Misri na Morocco zitakuwa nchi za kwanza za Afrika kujimwaga uwanjani Juni 15, Misri ikipambana na Uruguay katika mechi za kundi A, wakati Morocco itagongana na Iran katika mechi za kundi B siku hiyo hiyo ya Juni 15.
Makundi kamili ya Kombe la Dunia 2018
Kundi A: Russia, Saudi Arabia, Misri, Uruguay
Kundi B: Ureno, Spain, Morocco, Iran
Kundi C: Ufaransa, Australia, Peru, Denmark
Kundi D: Argentina, Iceland, Croatia, Nigeria
Kundi E: Brazil, Switzerland, Costa Rica, Serbia
Kundi F: Ujerumani, Mexico, Sweden, South Korea
Group G: Ubelgiji, Panama, Tunisia, Uingereza
Group H: Poland, Senegal, Colombia, Japan