Wakati akimteua Mugabe, Mkurugenzi mkuu mpya wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliisifia Zimbabwe kwa namna inavyozingatia afya ya umma. Lakini baada ya kupata malalamiko WHO ilitengua uteuzi huo.
Katika hatua yenye utata Jumamosi WHO ilimteuwa Mugabe katika nafasi hiyo ili kusaidia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile mshtuko wa moyo, kiharusi na pumu.
Mkurugenzi mkuu huyo ambaye ni mwafrika wa kwanza kuongoza idara hiyo ya Umoja wa Mataifa amekosolewa vikali na wapiga kampeni wa kimataifa wa haki za binadamu pamoja na wanaharakati wengine kwa kufanya uteuzi huo.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa U.N Watch, Hillel Neuer ameishutumu serikali ya Robert Mugabe kwa kuwakandamiza wanaharakati wa haki za binadamu, inapinga demokrasia na kuligeuza taifa hilo lililopo Afrika na mfumo wake wa afya kuingia katika hali mbaya ya kiuchumi.
BBC imeripoti kuwa serikali ya Uingereza inasema, imeshtushwa na kuvunjika moyo, kuwa shirika la Afya Duniani, WHO, limemtaja rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kuwa balozi wa nia njema.
Msemaji mjini London, alieleza kuwa Mugabe anakabiliwa na vikwazo vilivyowekwa na Marekani na Umoja wa Ulaya, na kuteuliwa kwake, kutaathiri kazi za WHO.