WHO yasema yapata ugumu kuchunguza homa ya mafua ya ndege

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus

Shirika la Afya Duniani linasema uwezo wake wa kutathmini na kudhibiti hatari inayoletwa na homa ya mafua ya ndege ya H5N1 ulimwenguni kote unapata ugumu kutokana na ufuatiliaji mdogo wa maambukizi ya wanyama na wanadamu ya ugonjwa huo.

Katika kikao na wanahabari katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, anasema Marekani wiki iliyopita iliripoti kisa cha nne cha binadamu kufuatia ng'ombe wa maziwa walioambukizwa.

Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vinasema mgonjwa huyo alikuwa mfanyakazi wa uzalishaji maziwa ambapo ng'ombe walipimwa na kukutwa na virusi hivyo.

Mtu huyo alikuwa na dalili chache, alitibiwa na kupona. Hakuna maambukizi ya virusi hivyo kutoka kwa binadamu hadi kwa binadamu yaliyoripotiwa.

Tedros amesema Cambodia pia iliripoti maambukizi mawili kwa watoto ambao walikutana na kuku welioambukizwa au kufa.