WHO inataka hatua zichukuliwe kukabiliana na magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa

Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani alipowasili kwa ajili ya CHOGM mjini Kigali

Januari 30 ni siku ya kimataifa ya Magonjwa ya Kitropiki yaliyopuuzwa, Shirika la Afya Duniani linataka hatua zichukuliwe kukabiliana na magonjwa haya ya kudhoofisha, ambayo yanawaathiri takriban watu bilioni 1.65 ulimwenguni.

Kundi la vimelea 20 na bakteria katika magonjwa ya kitropiki yameainishwa kuwa yamepuuzwa. Hii ni kwasababu yanawaathiri watu ambao wanaishi katika hali ya umasikini, jamii za ndani kabisa na hawako katika orodha ya kipaumbele cha afya duniani.

Ibrahim Soce Fall ni mkurugenzi wa WHO katika idawa ya Magonjwa ya Kitropiki yaliyopuuzwa, anasema magonjwa haya yanasambazwa na wadudu katika maeneo yenye ukosefu wa maji safi, huduma za vyoo na fursa ya huduma za afya. Anasema pia yanasambaa kwa njia ya chakula na maji ambayo si salama.

Fall anasema yanasababisha maafa makubwa kwasababu ya matokeo yake ambayo yana uharibifu na kulemaza.

“Kama ukiyachukulia magonjwa haya kama vile unajua ‘river blindness’ kwasababu yanaweza kupelekea upofu. Na hivyo hivyo ni sawa kama Trachoma. Kwahiyo, haya ni magonjwa mengi ambayo ni hatari na yana athari mbaya sana,” anasema Fall.

Trachoma ni ugonjwa wa macho ambao unaweza kusababisha upofu wa kudumu.

Fall anasema kuwa magonjwa haya hayavutii kiwango cha uwekezaji kinachohitajika kwa fursa za huduma za afya au kuendeleza nyenzo mpya kwa ugunduzi, matibabu, na chanjo.

Anaelezea kuwa baadhi yamagonjwa haya yamekuwepo kwa muda mrefu sana. Kwa mfano, magonjwa yaliyotajwa katika biblia, kama ukomaa, bado yapo katika nchi 139 na dengue, ambayo imekuwepo kwa takriban miaka 800, bado yameenea katika mataifa 129.

Licha ya changamoto nyingi, maendeleo yamepatikana katika kutokomeza NTD's. WHO inaripoti kuwa idadi ya watu wanaohitaji matibabu ya NTD's ulishuka kwa milioni 80 kati ya mwaka 2020 na 2021. Imegundua kuwa nchi 47 zimetokomeza walau NTD moja na nchi zaidi ziko katika utaratibu wa kufanikisha lengo hili.

Kwa mujibu wa Carter Center, kulikuwa na kesi 13 za ugonjwa wa Guinea Worm mwaka jana, kuusukuma ugonjwa kukaribia kutokomeza kabisa. Kituo hicho chenye makao yake Atlanta ambacho kimeanzishwa na Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter na mke wake, Rosalynn Carter. Wakati kilipoanza kuongoza kampeni ya kimataifa ya kutokomeza Guinea Worm mwaka 1986, kulikuwa na takriban kesi milioni 3.5 katika kiasi cha nchi 21 barani Afrika na Asia.

Maafisa wa WHO wanasema lengo waliloweka ni kutokomeza walau ugonjwa mmoja wa Kitropiki katika nchi 100 ifikapo mwaka 2030 na hilo linaweza kufanikiwa. Jumuiya ya kisayansi ina nyenzo na ufahamu wa kuokoa maisha na kuzuia maafa. Lakini WHO inasema mataifa yanahitaji kuchukua hatua pamoja na kuwekeza katika kusaidia kutokomeza magonjwa haya mabaya.