WHO inapendekeza chanjo ya COVID kutoka Oxford na AstraZeneca itumike Afrika

Mkurugenzi wa kieneo wa WHO kwa Afrika, Matshidiso Moeti anabainisha chanjo hiyo inaonekana kuzuia kesi kubwa za COVID-19 kwa watu waliopo hospitali. Hivyo anasema matumizi yake yatakuwa faraja kubwa kwa hospitali na mifumo ya kutoa huduma za afya barani Afrika ambayo imeelemewa

Shirika la afya Duniani-WHO linasema chanjo ya virusi vya Corona ya Oxford na AstraZeneca inaweza kuokoa maisha na kupendekeza itumike hata katika nchi za kiafrika, ambapo kumekuwepo na aina tofauti za mzunguko wa COVID-19. WHO inaripoti maambukizi ya virusi vya corona milioni 3.7 ikiwemo takribani vifo laki moja.

Tangu kesi ya kwanza ya COVID-19 ilipotambuliwa huko Afrika takribani mwaka mmoja uliopita, virusi vya Corona ambavyo vinasababisha ugonjwa huo vimebadilika. Bara hilo hivi sasa linakabiliwa na aina tofauti za virusi ambavyo ni hatari zaidi na vinasababisha vifo.

WHO linasema nchi nane zimeripoti maambukizi ya juu ya aina mpya ya virusi vilivyogundulika kwanza nchini Afrika kusini, na nchi sita zimeshuhudia aina hiyo mpya ya virusi iliyogundulika nchini Uingereza.

Kufuatia mabadiliko hayo, Afrika kusini imesema wiki hii itasitisha matumizi ya chanjo ya AstraZeneca kwa sababu haifanyi kazi katika kuzuia maambukizi dhaifu na ya wastani.

Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa kieneo wa WHO kwa Afrika

Hata hivyo mkurugenzi wa kieneo wa WHO kwa Afrika, Matshidiso Moeti, anabainisha chanjo hiyo inaonekana kuzuia kesi kubwa za COVID-19 kwa watu waliopo hospitali. Kwa hiyo anasema matumizi yake yatakuwa faraja kubwa kwa hospitali na mifumo ya kutoa huduma za afya barani Afrika ambayo imeelemewa.