WHO inadai China ina taarifa muhimu kuhusu chanzo cha Covid-19

Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus .

Shirika la Afya duniani WHO limesema Alhamisi kwamba linaamini kwamba China ina data za kutosha kufichua chanzo cha janga la Covid-19, na kwa hivyo kuomba Beijing itoe kila taarifa ilizo nazo kuhusiana na suala hilo.

Kiongozi wa WHO Tedro Adhanom Ghebreyesus amesema kwamba bila kufichuliwa kwa taarifa zote zilizopo na China, uchunguzi uliopo hauwezi kukamilika. Ikiwa zaidi ya miaka 3 tangu kutokea kwa janga la Covid-19, mjadala mkubwa ungali unaendelea ili kubaini chanzo chake.

Suala hilo limeleta utata miongoni mwa jamii ya wanasayansi pamoja na taasisi tofauti za Marekani, baadhi wakisema kwamba maradhi hayo yalianzia kwa wanyama na kuingia kwa wanadamu, huku wengine wakiamini kwamba yalianza kwenye maabara moja mjini Wuhan China, suala ambalo China imeendelea kukanusha.