Serikali za Uingereza na Ufaransa kwa miaka mingi zimejikakamua kuzuia wahamiaji wanaolipa maelfu ya euro kwa walanguzi kila mmoja, ili kuingia Uingereza kupitia bahari kutoka Ufaransa wakitumia boti dogo. Mamlaka za bahari zimesema Jumamosi kuwa kumekuwa na majaribio mengi ya wahamiaji kufanya safari hiyo hatari kwa kutumia boti katika siku za karibuni, wakati zaidi ya wahamiaji 200 wakiokolewa ndani ya saa 24 kuanzia Ijumaa hadi Jumamosi.
Takriban wahamiaji 12 wengi wakitokea Eritrea walikufa karibu na ufukwe wa Ufaransa, baada ya boti yao iliokuwa imebeba darzeni ya wahamiaji kuzama mwezi huu. Huo ndiyo mkasa mbaya zaidi mwaka huu uliofikisha jumla ya wahamiaji 37 waliokufa kwenye lango hilo la bahari, kulinganishwa na 12 waliokufa mwaka jana.
Zaidi ya wahamiaji 22,000 wamewasili Uingereza kupitia lango hilo tangu mwanzoni mwa mwaka, kulingana na maafisa wa Uingereza. Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, mwaka huu waliahidi kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na ongezeko kubwa la wahamiaji wanaoingia kwenye mataifa yao.