WFP yataka usalama kwa wasambaza chakula GAZA

Shirika la mpango wa chakula duniani (WFP), Jumanne limetoa mwito kuanzishwa kwa njia maalumu ya misaada ya kibinadamu ukanda wa Gaza na kutoa wito wa kuwepo na uhakikisho wa usalama kwa wafanyikazi wake.

Katika taarifa yake, WFP imesema imeanzisha operesheni ya dharura ya kutoa misaada ya chakula kwa zaidi ya watu 800,000 wa Gaza na Ukingo wa Magharibi ambao wanakosa huduma ya chakula, maji, umeme na mahitaji muhimu.

Shirika hilo la chakula limesema limesambaza chakula kilicho tayari kwa watu 73,000 ambao wako katika makambi ya Gaza.

WFP inasema ina wasiwasi kuhusu upatikanaji wa chakula katika maduka ya ndani huku chakula kikianza kuisha baada ya Israel, kutangaza kuzingira kabisa eneo la Palestina, Jumatatu.

Israel imesema ilikuwa ikijibu mashambulizi ya Jumamosi ya Hamas. Mipaka na vituo vya ukaguzi kati ya Gaza na Israel vimefungwa, jambo ambalo WFP inasema linazidisha mgogoro kwani inazuia misaada kuingia.