Mara ya mwisho kwa msafara wa chakula kufika katika mji mkuu wa Tigray, Mekelle, ilikuwa katikati ya mwezi Desemba. Mamilioni ya watu waliokumbwa na njaa kali katika jimbo ambalo limegubikwa na mzozo wamekuwa hawana chakula tangu wakati huo.
Katika onyo kwa pande zote zinazopigana na jumuiya ya kimataifa, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Tomson Phiri anasema idara ya shirika hilo ya huduma za kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia inakaribia kusitisha kabisa shughuli zake. Anasema mapigano makali katika eneo hilo yanazuia upitishaji wa mafuta na chakula.
“Akiba ya lishe lenye virutubsho kwa ajili ya matibabu kwa watoto wenye utapiamlo na wanawake hivi sasa imepungua, na nafaka za mwisho wa WFP, vyakula vingine na mafuta vitasambazwa wiki ijayo. Kwa sababu ya mapigano, ugawaji chakula uko katika kiwango cha chini mno kuwahi kutokea. Wafanyakazi wa misaada wa WFP walioko huko wamenieleza kwamba ghala ziko tupu kabisa,” anasema Phiri.
Mapigano yalizuka kati ya wanajeshi wa serikali ya Ethiopia na majeshi ya Tigray Novemba mwaka 2020. Hali imezidi kuwa mbaya sana tangu wakati huo. Shirika la Mpango wa Chakula linasema watu milioni 9.4 kaskazini mwa Ethiopia hivi sasa wanahitaji msaada wa chakula, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 2.7 kutoka miezi minne iliyopita.
Huko Tigray peke yake, Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 5.2 wanategemea msaada wa kimataifa ili kuishi. UN inasema watu 400,000 wanaishi katika hali ya njaa na wengine milioni 2 wanakaribia kukumbwa na njaa kali.
WFP inalenga kutoa chakula cha msaada kwa watu milioni 2.1 huko Tigray na msaada wa ziada kwa watu milioni 1.1 katika mikoa ya Amhara na Afar. Hata hivyo, fedha hakuna. Shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa limetoa ombi la haraka la msaada wa dola milioni 337 kufanya shughuli zake za program za dharura za chakula kaskazini mwa Ethiopia katika kipindi cha miezi sita ijayo.