Waziri wa serikali ya Afrika Kusini na walinzi wake waibiwa katika shambulio lisilo la kawaida

Polisi wa kitengo cha kuchunguza miili wakisimama karibu na gari zao kwenye tukio la mauaji ya kufyatulia risasi watu wengi, katika mji wa Gqeberha Afrika Kusini, Januari 29, 2023.

Polisi wa Afrika Kusini wamesema waziri wa serikali ameibiwa na walinzi wake kuibiwa bunduki katika kile maafisa katika nchi hiyo inayokumbwa na uhalifu wamekielezea kuwa “tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa”.

Shambulio hilo lilifanyika jana Jumatatu wakati waziri wa uchukuzi Sindisiwe Chikunga akisafiri kwenye barabara kuu kusini mwa Johannesburg, polisi wamesema.

“Tairi za gari la waziri zilitobolewa na misumari, na hivyo kusababisha gari lake kusimama na kupelekea wahalifu kuwaibia watu waliokuwa ndani ya gari hilo,” taarifa ya wizara ya uchukuzi imesema.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa waziri na walinzi wake walinusurika katika shambulio hilo “bila kujeruhiwa wakiwa salama.” Msemaji wa polisi Athlenda Mathe amesema majambazi hao walitoroka na mali binafsi ya waziri na walinzi wake pamoja na bastola mbili za jeshi la polisi la Afrika Kusini.