Waziri wa mambo ya nje wa Russia, atembelea Mali

Waziri wa mambo ya nje wa Russia, Sergei Lavrov

Waziri wa mambo ya nje wa Russia, Sergei Lavrov, amewasili Mali, Jumatatu jioni kwa mazungumzo na viongozi wa kijeshi wanaotaka msaada wa Moscow katika kupambana na uasi wa Kiislamu ambao bado umejikita licha ya mapigano ya miaka kadhaa. 

Ziara hiyo ya chini ya saa 24 imekuwa ya tatu ya Lavrov barani Afrika tangu Julai, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupanua uwepo wa Russia katika bara hilo huku kukiwa na hali ya kutengwa kimataifa tangu uvamizi wa Moscow nchini Ukraine mwaka jana.

Tangu kuchukua udhibiti wa Mali katika mapinduzi mawili tangu Agosti 2020, utawala wa kijeshi unaoongozwa na Kanali Assimi Goita umekubali uungwaji mkono wa Russia kusaidia mapambano yake dhidi ya jihadi baada ya kuwafurusha wanajeshi wa mtawala wa zamani wa kikoloni Ufaransa.

Maafisa kadhaa wa Mali wamesafiri hadi Moscow, lakini ziara ya Lavrov ni ya kwanza ya aina yake yenye lengo la kuimarisha nguvu mpya kwa usalama na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Mali.

Lavrov atafanya mazungumzo na Goita na mwanadiplomasia wake mkuu Abdoulaye Diop, huku mkutano na waandishi wa habari ukipangwa kufanyika baadaye.

Mali tayari imepokea ndege na helikopta za kushambulia kutoka Russia pamoja na mamia kadhaa ya wanajeshi wa Russia walioelezewa na viongozi wa Mali kuwa wakufunzi wanaosaidia kuimarisha ulinzi na uhuru wa Mali.

Maafisa wa nchi za Magharibi na baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema wapiganaji hao kwa hakika ni wanamgambo wa kundi la Wagner, ambao wameshutumiwa kufanya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu kwingineko barani Afrika.