Waziri wa afya wa Afrika kusini, Joe Phaahla alisema leo Ijumaa kwamba Afrika kusini inakabiliwa na wimbi la nne la maambukizi ya COVID-19, yanayotokana na aina mpya ya kirusi cha Omicron ambacho kimegundulika katika majimbo saba, kati ya tisa ya nchi hiyo.
Omicron ambayo imeibua khofu kimataifa ya kuongezeka kwa maambukizo, iligunduliwa kwa mara ya kwanza kusini mwa Afrika, mwezi uliopita na kusababisha serikali nyingi katika mabara yote kusitisha safari na kuchukua hatua nyingine za kujaribu kuzuia maambukizi kuenea.
Phaahla aliwaambia waandishi wa habari kwamba anatumai kuwa aina hiyo mpya ya kirusi kinaweza kudhibitiwa bila kusababisha vifo vingi. Alitoa wito kwa wa-Afrika kusini kupata chanjo kamili, na kuongeza kuwa nchi inaweza kudhibiti wimbi la nne bila kuwepo masharti ya kufunga huduma za jamii wakati wa sikukuu ya Krismas.