Waziri mkuu wa zamani wa Italy Silvio Berlusconi amefariki dunia, akiwa na umri wa miaka 86. Tajiri huyo biliyonia ambaye alikuwa anamiliki vyombo kadhaa vya habari, amekuwa akitibiwa ugonjwa wa saratani ya damu.
Berlusconi alianza kutengeneza utajiri wake katika sekta ya ujenzi wa majumba kisha akaendelea kuunda mtandao wa vituo vya televisheni, akifanikiwa sana katika biashara hiyo.
Wakati fulani, alijulikana kama tajiri mkubwa wa Italy.
Mwanasiasa huyo wa mrengo wa kulia alihudumu kama waziri mkuu katika serikali nne kuanzia mwaka wa 1994.
Berlusconi alikabiliwa na kashfa nyingi za kisiasa wakati wa maisha yake. Alijulikana kwa karamu zake mashuhuri za bunga bunga kuhusiana na kufanya ngono na makahaba, lakini kashfa hizo hazikumuzuia kujenga urithi wa kudumu wa kisiasa.