Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, Jumatano ametetea uamuzi wa serikali yake wa kusitisha kupelekwa kwa baadhi ya shehena za silaha kwa Israel, akisema hatua hiyo ni muhimu ili kufuata sheria za kimataifa.
“Tunatambua kabisa na kuunga mkono haki ya Israeli ya kujilinda na tumechukua hatua kuunga mkono haki hiyo, lakini swala hili linahusiana na leseni na si suala la Israeli,” amesema.
Ameongeza kusema mfumo wa leseni zote unapaswa kuangaliwa. Starmer amesisitiza kwamba nchi yake inafuata sheria za kimataifa na kuzitii.
Akiwa ndani ya bunge amegusia kwamba nguvu na hoja zao ni kwa sababu ya kufuata sheria za kimataifa. Israel imekosoa vikali hatua hiyo na kusema itatumiwa kuwaimarisha wanamgambo wa Hamas wa Gaza.
Israel ilivamia ardhi ya Palestina baada ya wanamgambo wa Hamas kuua zaidi ya watu 1,200 na kuwachukua mateka 253 katika shambulizi la kigaidi la kuvuka mpaka la 7 Oktoba.