Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok alitangaza Alhamis kuundwa kwa serikali ya kwanza tangu kuondolewa madarakani mwezi April, mtawala wa muda mrefu nchini humo Omar Hassan Al-bashir.
Serikali iliyoundwa ni sehemu ya mkataba wa miaka mitatu wa kushirikiana madaraka uliotiwa saini mwezi uliopita kati ya jeshi, vyama vya kiraia pamoja na makundi ya waandamanaji. Hamdok alitangaza majina ya mawaziri 18 katika baraza jipya la mawaziri na alisema kwamba atatangaza majina mawili zaidi baadae.
Hamdok aliwaambia waandishi wa habari mjini Khartoum kuwa serikali hiyo mpya itaanza kufanya kazi mara moja ikifuata misingi ya makubaliano yaliyoafikiwa. Baraza hilo la mawaziri linajumuisha wanawake wane akiwemo Asmaa Abdallah anayekuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa wa waziri wa mambo ya nje wa Sudan.
Nafasi ya waziri wa fedha imechukuliwa na Ibrahim Elbadawi, mchumi wa zamani katika benki ya Dunia. Madani Abbas Madani, kiongozi wa ushirika wa kiraia ambao ulipigia debe mkataba wa mpito na jeshi amepewa nafasi ya waziri wa viwanda na biashara.