Waziri mkuu wa Israel aapa kuendelea na vita dhidi ya Hezbollah

  • VOA News

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Alhamisi alisema kwamba Israel inapanga kuendelea kushambulia Hezbollah nchini Lebanon “kwa nguvu zote” hadi pale wakazi wa kaskazini mwa Israel watakaporudi majumbani kwao Salama.

“Hatutasitisha hadi tufikie malengo yetu, lengo kuu miongoni mwa hayo ni kuwarejesha wakazi wa kaskazini majumbani kwao kwa usalama,” Netanyahu aliwambia waandishi wa habari baada ya kuwasili Marekani, kabla ya kulihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa leo Ijumaa.

Muda mfupi kabla ya taarifa yake, jeshi la Israel lilisema lilimuua kamanda wa Hezbollah aliyesimamia ndege zisizo na rubani katika shambulizi la anga kwenye jengo la makazi katika vitongoji vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

Watu wawili waliuawa na wengine 15 kujeruhiwa katika shambulizi hilo, wizara ya afya ya Lebanon ilisema.

Netanyahu amethibitisha kuendelea kufanya mashambulizi nchini Lebanon huku maafisa wa Marekani na Ulaya wakishinikiza sitisho la mapigano kwa siku 21 kati ya Israel na Hezbollah ili mazungumzo yaweze kufanyika.

Lakini mapema Alhamisi, waziri wa mambo ya nje wa Israel Katz alitupilia mbali pendekezo hilo la kusitisha mapigano kwenye mpaka kati ya Israel na Lebanon.