Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed leo Jumanne alilitaka kundi la upinzani la Tigrayan kujisalimisha akidai kuwa wanajeshi wa serikali wanakaribia kupata ushindi wiki moja tu baada ya kwenda kwenye mstari wa mbele wa vita kuongoza operesheni za kijeshi.
Vijana wa Tigray wanaangamia kama majani. Wakijua kwamba wanashindwa, wanaongozwa na mtu ambaye hana mtazamo au mpango ulio sahihi, Abiy mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobeli mwaka 2019, alisema katika matamshi yaliyorushwa kwenye vyombo vya habari vya serikali.
Ameendelea kuandika kwamba wapinzani wanapaswa kujisalimisha leo kwa jeshi la ulinzi la kitaifa la Ethiopia, kwa kikosi maalum, kwa wanamgambo na kwa watu.
Picha za leo Jumanne zilikuwa za karibuni katika mifululizo ya video zinazomuonyesha Abiy akiwa amevalia sare na wanajeshi katika kile kinachoonekana kuwa wapo katika jimbo la kaskazini mashariki la Afar. Jimbo hilo limekuwa eneo la mapigano makali katika wiki za karibuni, huku kundi la wapinzani la Tigray People’s Liberation Front (TPLF), likijaribu kuchukua udhibiti wa barabara kuu inayoelekea mji mkuu Addis Ababa.