Waziri Mkuu mpya Libya aahidi kushirikiana na wananchi wote

  • Abdushakur Aboud

Abdul Hamid Mohammed Dbeibah, kamu Waziri Mkuu wa Libya akilihutubia taifa Jumamosi Februari 6, 2021

Kaimu waziri mkuu mpya wa Libya Abdul Hamid Dbeibah atoa ahadí ya "kuwa tayari kuwasikiliza na kufanya kazi na wananchi wole wa Libya," alipolihutubia taifa kwa mara ya kwanza Jumamosi usiku, Februari 6, 2021.

Abdul Hamid Dbeibah, mhandisi mwenye umri wa miaka 61, aliteuliwa Ijuma na Baraza la wajumbe 75 wa Libya, wakati wa mazungumzo yaliyoongozwa na Umoja wa Mataifa nje ya mji wa Geneva, ili kua kaimu waziri mkuu.

Mazungumzo hayo yanakamilisha utaratibu wa majadilinao yaliyoanza mwezi Novemba mwaka 2020 kwa lengo la kurudisha amani katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Kuanzia Jumamosi Libya imeanza awamu mpya ya mpito wa utawala, baada ya enzi ya Ghadafi, utakao ongozwa na utawala wa mpito uloteuliwa kutayarisha uchaguzi mkuu mwezi Disemba baada ya karibu muongo mmoja wa ghasia na mapigano.

Chini ya makubaliano hayo, yanayoleta mabadiliko makubwa na kuungwa mkono kwa tahadhari na mataifa makuu ya dunia, jopo la viongozi wanne kutoka maeneo ya magharibi, mashariki, kusini na kaskazini ya taifa hilo, wana jukumu kubwa la kuliunganisha tena taifa hilo tajiri la mafuta lililogawika kutokana na mivutano ya utawala wa pande mbili zilizokua zikihasimiana na makundi mengi ya wanamgambo.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa kama waziri mkuu, Dbeibah ametoa wito wa kuikarabati nchi hiyo na kuahidi "kua tayari kusikiliza na kufanya kazi na wa Libya wote", bila ya kujali nadharia, au kundi gani wanaunga mkono au jimbo gani wanakotoka.

Hotuba hiyo inachukuliwa kama ukurasa wa kwanza mpya wa mageuzi nchini Libya baada ya kushindwa kwa makubaliano ya kwanza yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015, yaliyoanzisha serkali ya Umoja wa Mataifa GNA iliyoongozwa na Fayez al-Sarraj.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "Nina amini ni maendeleo makubwa".

wakazi wa mji wa Tripoli wanaeleza furaha yao kutokana na mabadiliko hayo mepya wakiwa na matumaini ya kushuhudia mabadiliko ya kweli.