Wavuvi, wakulima na wachungaji wazozana Cameroon

Wanajeshi wa Cameroon washika doria kwenye picha ya awali kaskazaini mwa nchi

Mapambano  kati ya wakulima, wafugaji na wavuvi kutokana na uhaba wa maji kwenye mpaka wa kaskazini mwa Cameroon karibu na Chad yanasemekana kuongezeka sana katika siku za karibuni. 

Maafisa wa serikali kwa upande wao wanasema kwamba vijiji na masoko yalichomwa moto Jumatano huku maelfu ya wakazi wakilazimika kukimbilia nchi jirani ya Chad.

Mjumbe aliyetumwa na watawala wa kijadi kwa wakazi takriban 120 kwenye mji wa kaskazini mwa Cameroon wa Kousseri amewaambia kwamba bila amani hakuna maendeleo yatakayopatikana, na kwamba umaskini utaendelea kuwepo. Ameongeza kuwaambia kwamba ghasia zitaongeza hali ya njaa pamoja na mateso kwa wakazi.

Ujumbe huo umekuwa ukirudiwa mara nyingi kwenye chombo cha habari cha serikali cha CRTV kinachorusha vipindi kwa lugha za Massa, Mousgoum na Arab Choua. Jamii za Massa, Mousgoum na Arab Choua zinazoishi kwenye maeneo ya Logone na Chari, uliko mji wa Kousseri.

Maafisa wa serikali kwenye eneo la Logone na Chari wanasema kwamba walianza kueneza ujumbe wa amani baada ya ghasia kuzuka kati ya wakulima, wafugaji na wavuvi kutokana na uhaba wa maji.

Viongozi wa kijamii wamesema kwamba vijiji kadhaa vilichomwa pamoja na mashamba kuharibiwa huku soko kubwa la Kousseri likichomwa pia. Taarifa zimeongeza kusema kwamba zaidi ya watu 40 wameuwawa huku wengine 70 wakijeruhiwa na maelfu kulazimika kutorokea kwenye nchi jirani ya Chad.

Gavana wa eneo la kaskazini mwa Cameroon ambako vijiji vya Logone na Chali vinapatikana Midjiyawa Bakari, amesema kwamba aliongoza ujumbe wa maafisa wa juu serikalini pamoja na jeshi kufuatia amri ya rais Paul Biya kwenye vijiji hivyo.


Amesema kwamba rais angependa kuona jamii hizo zikiweka tofauti zao kando, kwa ajili ya kutafuta amani. Bakari amesema kwamba ghasia hizo huenda zikawazuia maelfu ya mashabiki wa soka kutoka kwenye mataifa jirani ya Chad, Sudan, Niger na Libya kuhudhuria kombe la mataifa ya Afrika litakaloanza Januari 9.