Wavuti 55 zimefungwa kwa kuonyesha kombe la dunia bila idhini

Mchezaji wa Uingereza Harry Kane baada ya Uingereza kubanduliwa kwenye michuano ya kombe la dunia

Jumla ya wavuti 55 ambazo zimekuwa zikionyesha michuano ya kandanda ya kombe la dunia yanayoendelea Qatar, bila kuwa na idhini, imefungwa na mamlaka nchini Marekani.

Wizara ya sheria imesema kwamba hatua ya kufunga wavuti hizo imechukuliwa baada ya mwakilishi wa shirikisho la kandanda duniani FIFA, kutambua wavuti ambazo zinatumika kuonyesha mashindano hayo ya mpira bila idhini ya shirikisho hilo.

Shirikisho la kandanda FIFA, ndilo lenye haki miliki za mashindano ya kombe la dunia, ambayo yamefikia hatua ya nusu fainali.

Mjumbe maalum wa wiizara ya usalama wa ndani ya Marekani James Harris amaesema kwamba japo watu wengi huenda wana Imani kwamba wavuti kama hizo sio tishio kubwa, ukiukwaji wa haki miliki ni tishio kubwa kwa ukuaji wa uchumi na kwamba athari zake zinaweza kuchangia kutokea kwa aina tofauti za uhalifu.

Wizara ya sheria ya Marekani hata hivyo haijataja wavuti ambazo zimefungwa lakini imesema kwamba watakaotembelea wavuti hizo wataelekezwa kwa wavuti tofauti kwa maelezo zaidi.