Waukraine wakimbia mapigano licha ya Russia kuziba njia za kuondokea

Wakimbizi wa Ukraine wanaokimbia uvamizi wa Russia nchini mwao wakisubiri kupanda basi linaloelekea mjini Przemysl, baada ya kuvuka mpaka wa Ukraine-Poland, Medyka, Poland, April 1, 2022. REUTERS/Hannah McKay

Maelfu ya Waukraine wamekimbia mapigano ya kikatili katika baadhi ya vituo muhimu wanavyoishi watu wengi vya nchi hiyo Ijumaa licha ya tatizo la kuwepo njia za dharura zilizowekwa awali kuwasaidia watu kuondoka.

Afisa mwandamizi wa Ukraine alisema jumla ya watu 6,266 waliweza kuondoka na kukimbia vita, ikiwemo zaidi ya watu 3,000 kutoka katika eneo lililozingirwa kusini mwa mji wa Mariupol.

Kukimbia kwa raia wengi kutoka Mariupol kulitokea hata pale jaribio liliposhindikana kuwaondoa watu wengi zaidi kutoka katika mji huo ambapo maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani walisema kuwa zoezi hilo lilizoroteshwa na mashambulizi ya anga na makombora yaliyofanywa na Russia.

Jaribio la kufikia mji huo kwa mabasi na kufika kwa waokoaji lilifeli baada “mipango na mazingira kufanya hilo lishindikane kuendelezwa,” Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundiu ilisema Ijumaa.

“Kwa operesheni hiyo kufanikiwa, ni muhimu kuwa pande hizo husika ziheshimu makubaliano na kuweka mazingira muhimu na kudhamini hali ya usalama,” Shirika la ICRC lilisema katika taarifa yake. “(Timu hiyo) itajaribu tena Jumamosi kurahisisha njia salama ya kupita raia kutoka mji wa Mariupol.”

Mapema Ijumaa, Gavana wa Mkoa wa Donetsk Pavlo Kyrylenko aliishutumu Russia kwa kuvunja ahadi ya kuruhusu njia za kibinadamu ambapo watu hawawezi kuondoka.

“Mahitaji ya kibinadamu, pamoja na makubaliano yote yaliyofikiwa na ahadi zilizotolewa na upande wa Russia, hazitekelezwi,” alisema wakati akitoa hotuba yake kwa njia ya televisheni.

Ripoti kutoka katika mkoa huo zinaonyesha kuwa wengi wa wale walioweza kukimbia kutoka Mariupol walitumia njia za kutembea kwa miguu.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema katika hotuba yake kwa njia ya video Ijumaa kuwa Ukraine inajadili pembeni “ kuondolewa kwa walioumia na wanajeshi wetu na raia waliouawa.” Amesema mazungumzo hayo yanafanyika Uturuki, ambayo inajukumu la upatanishi kati yao na Russia.

Ofisi ya Zelenskyy ilisema Ijumaa kuwa wanajeshi 86 wa Ukraine waliachiwa huru ikiwa ni sehemu ya hatua ya kubadilishana wafungwa na Russia. Haikuelezwa ni wanajeshi wangapi wa Russia waliachiwa huru.