Mgomo huo unaendelea kusambaratisha utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa katika hospitali za umma nchini Kenya.
Japo baadhi ya majimbo yameafikia muafaka na wauguzi kutoka majimbo hayo, maeneo mengine yangali yanakabiliwa na changamoto za utoaji huduma hizo.
Akizungumza na vyombo vya habari Ijumaa jijini Nairobi, Waziri wa Leba Ukur Yattani alieleza kuwa serikali itafika mahakamani Jumatatu kutaka mahakama iwaadhibu wauguzi hao kwa kutofuata wito wa kurejelea majukumu yao.
Sikiliza
Your browser doesn’t support HTML5
Jopokazi la kuondoa utata huo lililobuniwa na serikali limeonekana kutoafikia chochote kufuatia ususiaji wa wawakilishi wa wauguzi katika mazungumzo hayo huku wakiyataja kuwa yasiyokuwa na umuhimu wowote.
Muungano wa wauguzi nchini Kenya ungali unasisitiza kuwa wauguzi watarejelea majukumu yao tu wakati wizara ya afya na serikali za majimbo zitawalipa wauguzi malimbikizi yao.
Hata hivyo, Baraza la Magavana Alhamisi lilisisitiza kuwa ufuatiliaji wa amri ya Rais Kenyatta utafanyika Ijumaa kubaini wale wanaofika kazini.
Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini Kenya, COTU, sasa unamtaka Waziri Ukur Yattani kujiuzulu kwa "kumpotosha rais Kenyatta."
Francis Atwoli, Katibu Mkuu wa Muungano huo anasisitiza kuwa wafanyakazi wana haki ya kugoma.
Utata huu unafungamana na madai ya wauguzi kueleza kuwa serikali za majimbo zimejikokota kutoa mwongozo wa kutekeleza makubaliano ya kurejea kazini yalioafikiwa mnamo Novemba 2, 2017 kama njia ya kupiga marufuku mgomo wa wauguzi hao uliodumu kwa zaidi ya miezi mitano mwaka wa 2017.
-Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Mwandishi wa Sauti ya Amerika, Nairobi, Kenya.