Kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga aliandaa duru kadhaa za maandamano tangu mwezi Machi dhidi ya serikali, hali inayotia hofu jumuia ya kimataifa ambayo imejiunga na wito wa suluhu la kisiasa baada ya maandamano ya awali kusababisha vifo vya zaidi ya watu 10.
Mapambano kati ya polisi na waandamanaji yalisababisha vifo vya watu wawili katika ngome ya upinzani mjini Kisumu, alisema George Rae, mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga.
“Kuna miili miwili iliyorekodiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti ikiwa na majereha ya risasi, ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu, na kuongeza kuwa watu 14 wamelazwa hospitali.
Muungano wa Odinga wa Azimio uliapa kufanya maandamano kwa siku tatu mfululizo wiki hii, na Jumatano jioni uliwataka “Wakenya kujitokeza na kushiriki katika maandamano makubwa leo Alhamisi.
Licha ya maandamano ya Jumatano mjini Nairobi na katika miji mingine kuonekana yalidhibitiwa kuliko yale ya awali, na kukiwa ripoti chache kuhusu maafa kutokana na mapambano, waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki alisema maafisa wamerekodi visa vingi vya uharibifu na uporaji.
“Zaidi ya watu 300 walikamatwa nchini kote na watashtakiwa kwa makosa tofauti ya uhalifu, ikiwemo uporaji, uharibifu wa mali, uchomaji moto, wizi kwa kutumia nguvu, kushambulia maafisa wa usalama,” alisema Kindiki.