Watu wasipoungua 80, 000 wamepoteza makazi yao katika miezi mitatu ya ghasia za kikabila katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria afisa wa eneo hilo alisema wakati jeshi likiimarisha usalama ili kumaliza mapigano hayo.
Tangu mwezi Mei jimbo la Plateau limeshuhudia kuongezeka kwa mashambulizi hasa zaidi miongoni mwa Waislamu wafugaji wanaohamahama na jumuiya za wakulima wa Kikristo katika ghasia ambazo serikali ya jimbo hilo inasema zimesababisha takriban watu 300 kupoteza maisha.
Mkuu wa majeshi wa Nigeria Meja-Jenerali Taoreed Lagbaja aliitembelea Mangu katika Jimbo la Plateau Jumamosi kuashiria kuanza kwa operesheni maalum za kumaliza mzozo huo.
Mapigano hayo ni moja ya changamoto kuu za kiusalama zinazomkabili Rais mpya Bola Ahmed Tinubu nchini Nigeria ambapo wanajeshi pia wanapambana na wanajihadi magenge ya majambazi wenye silaha nzito na mivutano ya watu wanaotaka kujitenga.