Watu wanane wauawa kwa kupigwa na umeme nchini Afrika Kusini

Nguzo za umeme katika mji wa Soweto nchini Afrika Kusini

Watu wanane wakiwemo watoto wanne waliuawa kwa kupigwa na umeme katika matukio mawili tofauti baada ya siku kadhaa za mvua kubwa kusababisha mafuriko katika makazi duni karibu na mji wa Cape Town, idara ya huduma za dharura imesema Jumanne.

Nyumba nyingi katika vitongoj duni vya nje ya mji wa pili kwa ukubwa nchini Afrika Kusini vina umeme wa kuunganishwa, ambapo watu huunganisha wenyewe nyumba zao au vibanda kwenye waya za umeme zilizopo.

Waya hizo ni haramu na hatari, lakini zimeenea karibu mahali pote.

Kimbunga ambacho kilipiga eneo la mji wa Cape Town na sehemu kubwa ya mkoa wa Western Cape kwa siku tatu, na kusababisha mito kupasua kingo zake na mafuriko kwenye maeneo ya makazi na barabara kuu, kote katika mikoa ya pwani na bara. Mamia ya watu walihamishwa.

Zaidi ya wateja 80,000 katika mkoa wote hawakuwa na umeme kutokana na hali mbaya ya hewa ambayo ilisababisha umeme kukatika, mamlaka ya umeme imesema. Lakini baada ya mvua kupungua, idadi hiyo ilipungua na kufikia watu 15,000 ambao hawakuwa na umeme leo Jumanne.