Waziri wa Afya wa Msumbiji alisema Ijumaa kuwa mlipuko wa kipindupindu katika eneo lililopigwa na Kimbunga Freddy kimeua watu wanane wiki hii na wengine 250 wamelazwa hospitali – ikiwa ni sehemu ya watu 600 ambao ni wagonjwa tangu kutua kwa kimbunga katika eneo hilo mwezi Februari.
Waziri wa Afya Armindo Tiago amekiambia Radio Msumbiji inayomilikiwa na serikali kwamba waathirika wa kipindupindu walikuwa katika mji wa bandari wa Quelimane, mji mkuu wa Jimbo la Zambezia, eneo lililokuwa limeathiriwa sana na kimbunga hicho.
Tigao alisema hatua ya kuzuia kipindupindu imelengwa katika vituo 133 vya mji huo ambavyo vinatoa hifadhi kwa takriban watu 50,000 waliokoseshwa makazi kutokana na mafuriko. Ameongeza kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika majimbo mengine yaliyokumbwa na Kimbunga Freddy, kimbunga cha historia ambacho kimepiga katika eneo hilo tangu Februari.
Tiago alisema kila mtu lazima afanye juhudi kudhibiti mlipuko huo kwa kuchemsha maji ya kunywa, kusafisha na kuosha chakula, na kutupa takataka inavyotakiwa – hususan choo cha binadamu. Iwapo watu wana dalili kama vile kuharisha na kutapika, lazima wafike katika vituo vya afya.
Shirika la Afya Duniani Jumatano limethibitisha kuwa Msumbiji inashuhudia ongezeko la maambukizi ya kipindupindu, wakati idadi ya maambukizi hayo ikipungua katika nchi jirani ya Malawi baada ya kuwa na rekodi ya juu.
WHO ilisema zaidi ya maambukizi 40,000 ya kipindupindu yameripotiwa mwaka huu huko Afrika, na zaidi ya nusu yake nchini Malawi.