Kulingana na shirika la afya duniani WHO na shirika la kuangazia maambukizi ya virusi vya Ukimwi – UNAIDS, athari zitokanazo na matatizo ya kutoa dawa kwa wagonjwa wa ukimwi kwa mda wa miezi sita, zinaweza kudumaza kabisa mafanikio ambayo yamepatikana katika kuzuia vifo kutokana na Ukimwi.
Ripoti ya mashirika hayo imeonya kwamba idadi ya vifo kutokana na Ukimwi inaweza kuongezeka na kufikia ya mwaka 2008, ambapo watu 950,000 walikufa Afrika.
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO, Tedros Adhanon Ghebre-yesus, amesema kwamba “kuna uwezekano wa zaidi ya watu nusu milioni kufariki Afrika kutokana na ukimwi, na hali hiyo itakuwa mbaya sana”.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS Winnie Byanyima, ameonya kwamba mpango wa kutoa tiba kwa wagonjwa wa ukimwi unaweza kutatizika, kutokana na janga la Corona.
“kuna hatari ya mafanikio yaliyopatikana kufikia sasa katika vita dhidi ya Ukimwi kutozingatiwa kabisa, huku jihudi zote zikielekezwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona,” ameonya Wiinie Byanyima.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO, amesisitiza kwamba kuna umuhimu mkubwa katika kuhakikisha kwamba watu wanaopatikana kuambukizwa virusi vya ukimwi, wanapewa dawa.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.