Watu 6 wauwawa kwa kukatwa vichwa Msumbiji

Rais wa Msumbiji,Filipe Nyusi.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amesema Jumatano kwamba wanamgambo wa kiislamu kwenye jimbo la kaskazini la Nampula wameua watu 6 kwa kuwakata vichwa huku wengine watatu wakitekwa nyara.

Vunguvugu la wanamgambo kaskazini mwa taifa hilo linaendela kuenea kwenye maeneo mapya licha ya juhudi za serikali pamoja na vikosi vya kieneo za kulidhibiti. Wakati akizungumza mubashara kupitia televisheni ya kitaifa akiwa kwenye jimbo la kusini la Gaza, Nyusi amedhibitisha tukio hilo akiongeza kwamba darzeni ya nyumba pia zilichomwa.

Hilo ndilo shambulizi la tatu kufanyika mkoani Nampula ndani ya kipindi cha siku 5, hali ambayo imesababisha wimbi jipya la watu wanaotoroka makwao, ingawa idadi kamili haijulikani. Nyusi amesema kwamba imekuwa vigumu kwa vikosi vyake kuwasaka magaidi kutokana na kuwa wanajificha kwenye misitu mikubwa baada ya kufanya mashambulizi.

Kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi kwenye eneo la Cabo Delgado katika miaka ya karibuni, wakazi wengi wamelazimika kutorokea Nampula wakitafuta usalama. Mkoa huo sasa ni wa tatu kaskazini mwa Msumbiji kushambuliwa na magaidi baada ya Cabo Delgado na Niassa.